Thursday, August 23, 2012

LEO NDIO LEO BARCELONA Vs REAL MADRID



Kocha wa Barca Tito Vilanova

Kocha wa Real Madrid Jose Mourinho

TITO Vilanova alikuwa Barcelona kama msaidizi wa Pep Guardiola wakati alipotawala vichwa vya habari Agosti mwaka jana baada ya kuchapwa kibao cha usoni na kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho kwenye mchezo wa Hispania Super Cup.

Leo ni mwaka umepita tangu tukio hilo limetokea na Tito amechukua jukumu la rafiki yake la kuifundisha Barca sasa anakutana tena na Mourihno katika mchezo wake wa kwanza mgumu kama kocha utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nou Camp (saa 5:30 usiku).

Mabingwa watetezi Barca wamefuzu kucheza hatua hiyo baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mfalme na hiyo itakuwa mechi ya kwanza ya kupima ubora wa kikosi cha Vilanova dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu.

Uhasama baina ya wachezaji uliosabishwa na kadi tatu nyekundu kwa wachezaji wa Real mwaka 2011 pamoja na picha za televisheni kuonyesha Mourinho akimzaba kibao Vilanova umepungua kwa kiasi kikubwa.

Tukio hilo lilisababisha Mourinho kufungiwa mechi mbili za Super Cup, na Vilanova mechi moja kwa kuonyesha ishara mbaya, lakini adhabu hizo zote zimefutwa na rais wa shirikisho la soka la Hispania, Angel Maria Villar.

Mourinho, amekataa kuomba msamaha kwa yeyote, lakini mashabiki wa Madrid wamejitokeza na kukiriki kuwa kocha wao alifanya kosa.

Imeanza Ligi Vyema,
Barca imeanza vizuri kampeni zake za kusaka ubingwa wa ligi kuu kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Real Sociedad Jumapili iliyopita, huku wapinzani wake Real Madrid wakilazimishwa sare 1-1 nyumbani na Valencia.

Kuanza vizuri kwa Vilanova katika ligi kumechagizwa na kurejea kwa mshambuliaji wake David Villa aliyekuwa nje kwa zaidi ya miezi nane baada ya kuvunjika mguu, lakini Jumapili alifanikiwa kufunga bao kwenye ushindi wao mnono wa mabao matano.

Mshambuliaji huyo wa Hispania bado hajawa fiti na kuna uwezekano leo akapumzishwa kama itakavyokuwa kwa kiungo mpya Alex Song.

Mchezaji pekee mwenye uhakika wa kuanza leo ni Lionel Messi ambaye msimu uliopita alifunga mabao 73 ndiye atakayeongoza mashambulizi dhidi ya Real.

"Timu bado imebaki ile ile na falsafa na mtindo ni ule kama ilivyokuwa enzi za Guardiola," Messi aliimbia Barca TV.

"Bado wachezaji wote wanahamu ya kupata mataji. Nataka kushinda kila kitu na kocha Tito."

Kinara wa ufungaji wa Real, Cristiano Ronaldo bado hajawa fiti na katika mchezo wa kwanza wa ligi uliofanyika kwenye uwanja wa Bernabeu alishindwa kupiga hata shuti moja golini.

"Bado sijawa fiti kwa asilimia 100, lakini natumaini nitarudi kwenye kiwango changu haraka," alisema Ronaldo.

Mreno mwenzake Pepe ameondolewa kwenye kikosi kitachocheza mechi hiyo baada ya kuumizwa wakati alipogongana na kipa wake Iker Casillas kwenye mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Valencia.

Pamoja na Barca kutawala sana mechi za 'clasicos' chini ya Guardiola, lakini Real wamepoteza mechi moja tu wakiwa na Mourinho kati ya mara nne walizokutana Catalunya