Tuesday, June 12, 2012

EURO 2012 UINGEREZA YAKABANA KOO NA UFARANSA, UKRAINE YAISAMBARATISHA SWEDEN


Andriy Shevchenko akitupia kambani kwa kichwa goli la kwanza

Mwachemwache kati ya Ibrahimovic wa Sweden na Khacheridi wa Ukraine

Mtanange wa michuano kombe la mataifa ya Ulaya umeendelea kwa mtindo wa kipekee kwa wenyeji Ukraine kuishushia kichapo Sweden cha mabao 2-1, huku mshambuliaji matata Andriy Shevchenko 'Sheva' akifunga mabao yote mawili maridadi kabisa kukamilisha siku njema kwa waandaaji hao wenza wa michunao ya UEFA EURO 2012 katika kundi D.
Zlatan Ibrahimovic aliifungia Sweden goli la pekee dakika saba baada ya kipindi cha mapumziko. Kisha baadaye mchezaji nyota wa zamani wa timu ya Milan, Shevchenko mwenye umri wa miaka 35 aliwasazisha dakika tatu baada ya bao la Ibrahimovic na kisha kupachika bao la ushindi dakika ya 68 ya mchezo.


Schevchenko akitupia la pili


Schevchenko akishangilia msumari wa pili

Ibrahimovic akishangilia goli la kufutia machozi

Baada ya mechi hiyo Schevchenko alisema anahisi ni kama ana umri wa miaka 20 na wala sio 35. "Tuna nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hii. Najisikia vizuri. Ulikuwa mchuano wa kihistoria kwetu. Ni ushindi wa kihistoria," aliongeza kusema Schevchenko.
Kocha wa Sweden, Erik Hamren hajaridhishwa na matokeo hayo. Amesema ili kushinda mechi zao wanahitaji wachezaji 11 waonyeshe mchezo wa hali ya juu kabisa. "Leo pengine watano au sita walionyesha ujuzi ninaoutaka. Hiyo haitoshi," akaongeza kusema kocha huyo.
UKRAINE Vs SWEDEN


Ufaransa yatoka sare na England
Kwenye mechi ya kwanza ya kundi D, England ilitoka sare ya 1:1 dhidi ya Ufaransa. Mkwaju wa 'freekick' uliopigwa na Steven Gerrard baada ya mwenzake James Milner kufanyiwa madhambi na Patrice Evra wa Ufaransa, ulipachikwa wavuni na Joleon Lescott kwa kichwa dakika ya 30 ya mpambano huo. Samir Nasri aliutikisa wavu wa England na kusawazisha dakika chache baadaye.



Lescott akipiga ndosi iliyokwenda moja kwa moja kambani na kuipatia England bao la kuongoza

Bao la Nasri lilikuwa na umuhimu mkubwa zaidi kuliko kusawazisha tu kwa sababu limeisaidia Ufaransa kuepuka aibu nyengine baada ya balaa la michuano ya kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na michunao ya kufuzu kwa EURO 2008 ambapo wachezaji walirejea nyumbani wakiwa na aibu baada ya kutolewa kwenye raundi ya kwanza.
Nasri mwenyewe amesema ana imani wanayo nafasi nzuri katika michuano ya mwaka huu na lengo lao ni kufika robo fainali. "Hatujapoteza kwa hiyo ni muhimu kuzingatia mpambano wetu dhidi ya Ukraine siku ya Ijumaa."


Mwajiri wetu mmoja kaka adoadoo!!! ndivyo Nasri wa Ufaransa anavyomuambia mlinda mlango wa Uingereza Joe Hart ambae wanakipiga nae Manchester City 

mwachemwache kati ya Ashley Cole na Samir Nasri

Huendi popote hapa!!! Gerradi akimpiga mkwara Ribery

Kocha wa Ufaransa, Laurent Blanc, amesema hawajafurahishwa sana na matokeo ya mechi hiyo lakini hawajavunjika moyo. "Tungepoteza mechi hii kama hatungejitahidi, lakini ukiangalia kwa ujumla tumecheza vizuri zaidi kuliko England," ameongeza kusema kocha huyo. Naye kocha wa England, Roy Hodgson kwa upande wake amesema mechi ilikuwa ngumu lakini wameridhika na matokeo.
Ufaransa sasa itachuana na Ukraine ambayo iko katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa robo fainali huko Donetsk Ijumaa ijayo. England kwa upande wao wataumana na Sweden.
FRANCE Vs ENGLAND