Thursday, June 7, 2012

NAMBA YA BAHATI YA KELVIN YONDANI YAFYATUKA SIMBA YANGA WAMGOMBANIA


Kelvin Patrick Yondani akisaini mkataba na Yanga

Sehemu ya mkataba baina ya Yondani na klabu ya Yanga

Pamoja na mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kufunguka kuwa beki wa timu hiyo Kelvin Yondani ni mchezaji wao halali, klabu ya Yanga nayo imefunguka kivyake kwa kusema, ilimsajili beki huyo kwa Sh30 milioni. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema walimsajili rasmi Yondani Februari 20 mwaka huu.

Katika msimu uliopita Yondani aliingia katika mgogoro na klabu yake ya Simba kutokana na kutofautina na uongozi wa Simba."Yondani alimwaga wino wa kuichezea Yanga kwa mwaka mmoja na mkataba alisaini rasmi Februari 20 mwaka huu na utafikia kikomo Machi 20 mwaka ujao, ambapo atakuwa akipokea mshahara wa Shilingi 800,000,"alisema Sendeu.

Alisema,"Tumefuata taratibu zote zinazostahili za kumsajili mchezaji kwa mujibu wa kanuni na sheria za Fifa, tulizungumza naye miezi sita kabla ya ligi kumalizika mwezi Mei mwaka huu."

Sendeu alisema hawatakubali kuyumbishwa na vitisho vya uongozi wa Simba kwa kuwa, sheria zote wanazifahamu na wamezifuata na kama wakigundua kuwa kuna udanganyifu wowote umefanyika, basi watachukua hatua kali za kisheria bila kujali hadhi ya mtu.


Ofisa habari wa Dar Young Africans (Yanga) Louis Sendeu

Kauli ya Sendeu imekuja saa chache baada ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage kudai kuwa Yondani bado ni mchezaji wao halali na kwamba waliomsajili wanajisumbua na watawachukulia hatua za kisheria.

"Msimu uliopita tuliwapa tahadhari wasimsajili mchezaji wetu mmoja ambaye tulitaka kumsajili, lakini wakaendelea na harakati zao wakatumia nguvu kubwa na kupoteza fedha matokeo yake wakasajili bomu na sasa tunawatahadharisha waache hizo harakati zao wanazozifanya, Yondani bado ana mkataba wa mwaka mzima wa kuichezea Simba tutawashtaki," alisema Rage.


Mwenyekiti wa Simba Sports Club Ismail Aden Rage

Yondani ataingia kwenye orodha ya wachezaji, ambao wamewahi kuzisumbua klabu hizo mbili kwenye usajili wake akiwamo Victor Costa, Athuman Idd Chuji, Kenneth Asamoh ambaye awali alitaka kusajiliwa na Simba, lakini Yanga wakawapiga bao na jana Rage aliwapa dongo kuwa mchezaji huyo ni bomu.

Ndoto za Yondani kukipiga kwenye klabu ya Yanga msimu uliopita zilisababisha vuta ni kuvute ya muda mrefu kabla ya baba yake mzazi kuingilia kati na kumaliza mgogoro huo na kurejea tena kundini kukipiga kwenye timu ya Simba.

Sendeu alisema Yondani ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga watakaoingia kambini Juni 14 kujiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame pamoja na Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


Yondani kushoto akikabiliana na Tegete katika moja ya mechi za watani wa jadi Simba na Yanga

OKWI ANA THAMANI YA Tshs BILIONI 1


Emmanuel Okwi katika uzi wa Klabu yake ya Simba Sports

KLABU ya Simba imesema iko tayari kumruhusu mshambuliaji wake wa kimataifa toka Uganda, Emmanuel Okwi kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini hilo litawezekana iwapo klabu itakayomuhitaji itakubali kulipa ada ya uhamisho ya Pauni 500,000 (Sh1.3 Bilioni).

Okwi aliyetoa mchango mkubwa na kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Bara msimu huu, amepata ofa ya kwenda kufanya majaribio katika nchi tatu, Uingereza, Serbia na Austria.

Akiongea jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema kimsingi klabu yake imekubali maombi kutoka nchi hizo ili nyota huyo aende kufanya majaribio.

"Kwa kuzingatia sera ya klabu, tumekubali maombi hayo na tuko tayari kumruhusu Okwi kwenda kufanya majaribio wakati wowote atakapohitajika kufanya hivyo," alisema Rage.

"Kumekuwa na maneno mengi kuhusu Okwi, hapa napenda kutoa ufafanuzi sahihi kwamba, tumepokea maombi ya mawakala kutoka Uingereza, Serbia na Austria akihitajika kwenda kufanya majaribio," aliongeza.

Rage alisisitiza kuwa, klabu yake haina kinyongo na mchezaji huyo kwenda kucheza Ulaya, lakini kwa ada ya uhamisho inayokwenda sambamba na kiwango cha mchezaji huyo, ambacho ni Sh1.3 Bilioni.

Wolfgang Strainwender, wakala raia wa Austria ndiye ameonyesha kumuhitaji haraka Okwi baada ya kumwona kwenye mchezo kati ya Uganda na Angola uliokwisha kwa sare ya bao 1-1, huku bao la Uganda likitumbukizwa wavuni na Okwi, alifafanua Rage.

"Wakala wa Uingereza na Serbia hawajasema wanamuhitaji haraka kiasi gani. Nadhani kufikia kesho jioni tutakuwa kwenye nafasi ya kufahamu ni lini atakwenda Austria," alisema Rage.




Okwi akimwaga udambwidambwi na klabu yake ya Simba Sports

Okwi akiwa katika uzi wa Timu yake ya Taifa Uganda "The Cranes"

Wakati huohuo, Rage alisema kikosi chake kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam, Juni 15 kikiwa na wachezaji 25 kuelekea mkoani Shinyanga kwa ajili ya kucheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Toto Africans.

Alisema baada ya mechi hiyo msafara wa Simba utakwenda Mwanza ambako pia utacheza mechi nyingine ya kujipima nguvu Juni 17.

"Nichukue fursa hii pia kuwaambia wale wanaotaka kujua Simba imemsajili nani na kumwacha nani, kufikia Juni 15 watafahamu kila kitu kwani kikosi chetu kitakuwa na sura mpya," aliongeza Rage