Tuesday, April 3, 2012

MAN UNITED YAIFYATUA BLACKBURN 2-0

Manchester United imeendelea kujichimbia kileleni mwa ligi kuu ya England baada ya kuizaba Blackburn Rovers kwa mabao 2-0. Man United wakicheza ugenini walibanwa kwa takriban dakika 80.
Baada ya kulisakama lango la Blacburn kwa dakika 80,Antonio Valencia ndiye aliandika bao la kwanza la United baada ya kuachia mkwaju mkali kutoka upande wa kulia.

Antinio Valencia akishangilia baada ya kutupia kambani goli la kuongoza la Man U


Ashley Young akiachia 'fataki' na kuandika goli la pili

Dakika tano baadaye, Ashley Young aliyeingia badala ya Paul Scholes alifunga bao maridadi na kuhakikishia United pointi tatu muhimu katika mbio za kutetea ubingwa wao.
Blackburn imerejea katika nafasi ya kumi na nane.



DIVA AMCHANA WEMA, AFAGILIA DIAMOND KUWA NA JOKATE


LOVENESS LOVE "DIVA"

Mtangazaji wa kipindi cha ala za roho kupitia kituo cha redio cha Clouds FM 88.4 Loveness Love 'Diva' amefunguka na kumchana 'live' Msanii maarufu wa filamu za bongo Wema Sepetu kwa kile kilichoonekana kukerwa na tabia 'chafu' za msanii huyo.
Kupitia kipindi cha ala za roho ambacho huendeshwa mida ya usiku kupitia kituo cha Clouds FM Diva alikitumia kipindi hicho ipasavyo kumchana Wema baada ya kupatwa na mkasa wa kuachwa solemba katika show baada ya kuwekeana makubaliano kuwa Wema afanyiwe mahojiano 'interview' lakini hakutokea.

Loveness Love "DIVA" na mpenzi wake Mo Racka

Diva alifunguka huku akimshutumu Wema kwa kutojali kazi za wenzake"Yeye ni kazi yake na wenzake tupo kazini lazima abadilike aheshimu kazi za wenzake"Alisema Diva.
Diva alielezea kuwa baada ya Wema kutotimiza makubaliano alijaribu kumtafuta katika simu ya mkononi lakini Wema alikuwa hapokei ndipo alipompigia Meneja wa Wema ajulikanae kama Martin.
Diva anasema kuwa alichojibu Meneja huyo ni kuwa Wema ni mtu anaependa 'Drama na atention' akiwa na maana Wema ni mtu wa kupenda michezo ya kuigiza na kuwafanya watu wawe makini na nini kilichotokea ni kama aina ya mtu anaependa skendo hivi ili watu waweze kumfuatilia mara kwa mara.


Wema Sepetu

Diva alikasirishwa na tabia hiyo na kusema kuwa kama Wema ni mtu wa kupenda drama ndio maana Diamond amemmwaga,'kama ni kweli Diamond anatoka na Jokate namuunga mkono kwasababu hakuna mwanaume anaependa 'drama na attention' " alisema Diva.'
'Kama unapenda penda mtu kama Jokate' aliongeza Diva kwa kile kilichoonekana kumfagilia Jokate kuwa na Diamond na kumkejeli Wema kwa kupigwa chini.
Katika kuweka msisitizo Loveness Love Diva akaweka wimbo wa Dioamond "Nimpende nani?" na akaendelea kupiga vijembe akisema mpende Jokate. Hapa alinikumbusha show ya Diamonds are forever iliyofanyika pale Mlimani City ambapo baada ya kupigwa wimbo wa Diamond Nimpende nani,ukumbi ulilipika kwa shangwe na kila mtu akimtupia jicho Wema nahisi ndio kitu kinachoitwa drama na attention anachokipenda Wema,mwisho katika Wimbo wa nimpende nani mwisho kuna kibwagizo kinachosema "nani amenuuuna?" basi Diamond alipofika katika kibwagizo hicho watu ukumbini walikuwa wakiitikia "Wemaaaaa","nani amenuuna?"..."Wemaaaaaaa".


Diamond "rais wa wasafi"

Jokate Mwegelo

Diva hakuishia hapo ndipo alipoanza kuuchambua wimbo wa Barnaba "Magubegube". ikumbukwe Barnaba pia alikuwepo katika show ya Diamonds are forever,show ambayo Diva aliifagilia ile mbaya akisema hakika ni next level,"Elfu hamsini(50,000) na tiketi zimeisha watu wamejaa show baab kubwa" alisema Diva.

Diamond akimlisha Wema keki enzi za mapenzi yao

Diva alipoweka wimbo wa magubegube akasema" Usiombe ukutane na magubegube,Diamond amekutana nayo na sasa yanamsumbua lakini amesimama imara na wanaume wengi wamekutana nayo" Hii ni dhahiri kuwa ni vijembe kwa Wema na kumfananisha na Gubegube.
Jamani show ya Diamonds are forever ilikuwa ni baab kubwa elfu hamsini na tiketi zimeisha watu kibao show ya nguvu ni maneno ambayo Diva aliyarudia mara kwa mara akimfagilia Diamond na kusema kuwa amefungua milango kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya hapa bongo.

CCM YAANGUKIA PUA ARUMERU 'WHITE HAIR' CHALI


Mshindi wa kiti cha ubunge (CHADEMA) jimbo la Arumeru Joshua Nassari

NI Chadema. Tambo za muda mrefu za nani angeibuka mshindi katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki zilifikia kikomo jana, baada ya Chadema, kunyakua jimbo hilo.  Mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari aliibuka kidedea baada ya kupata kura 32,972 sawa na asilimia 54.91 ya kura halali 60,038 zilizopigwa katika vituo 327 vya kupigia kura jimboni humo.

Nassari alimbwaga aliyekuwa mshindani wake wa karibu, Sioi Sumari wa CCM, ambaye alipata kura 26,757 ambazo ni sawa na asilimia 44.56. Uchaguzi huo mdogo ulifanyika kufutia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari mwanzoni mwa mwaka huu.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo jana alfajiri, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi alisema watu waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 127,455 na waliojitokeza kupiga kura ni 60,699 sawa na asilimia 48.38 ambapo kura 661 zilikataliwa hivyo kufanya kura halali ziwe 60,038.

Kwa mujibu wa sura 343 ya sheria za uchaguzi nchini na kwa mamlaka niliyopewa namtangaza ndugu Nassari Joshua, kuwa mbunge wa jimbo hili la Arumeru Mashariki,alisema Kagenzi, kauli ambayo iliibua shangwe kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wakisubiri matokeo hayo usiku kucha kwenye kituo cha kujumlishia kura kilichopo katika mji mdogo wa Usa River.

Kagenzi aliwataja wagombea wengine ambao kwa ujumla wao walipata asilimia 0.53 ya kura zilizopigwa kuwa ni Abdalah Mazengo wa AFP aliyepata kura 139, Mohamad Abdalah Mohamed wa DP kura 77, mgombea wa SAUÂ Shabani Kirita aliyepata kura 22, Hamis Kieni wa NRA kura 35, wa TLP Abraham Chipaka kura 18 na mgombea wa UPDP, Charles Msuya alipata kura 18.

Idadi ya wapigakura waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo mwaka huu waliongezeka kwa asilimia 8.2 ikilinganishwa na wapigakura 55,698 waliojitokeza Oktoba 31, 2010 kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.Kadhalika kura zilizokataliwa zimepungua kutoka za mwaka juzi kura 1,297 hadi kufikia kura 661 katika uchaguzi wa juzi, sawa na asilimia 49.03.

Sioi, wenzake wakacha kusaini

Mgombea wa CCM, Sioi na wagombea wengine wawili wa vyama vya NRA na UPDP jana hawakujitokeza kusaini fomu za matokeo ya uchaguzi huo licha ya kuitwa mara kadhaa na msimamizi wa uchaguzi.

Awali Sioi, alifika katika chumba cha majumuisho ya kura saa 6:15 usiku akiwa ameandamana na Makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Beno Malisa na makada kadhaa wa CCM na mara baada ya kufika katika chumba hicho, walifanya mazungumzo kidogo na msimamizi wa uchaguzi.

Baadaye Sioi aliondoka na makada hao majira ya saa 7 usiku na kutokomea huku Malisa akieleza kuwa mgombea huyo wa CCM jana hakuwa tayari kutoa maoni kuhusu uchaguzi huo.Tunaomba mtuache kwanza, ila katika siasa kuna kushinda na kushindwa na mwanasiasa lazima atambue haya mawili, alisema Malisa.

Mkesha wa kusubiri matokeo
Wafuasi wa Chadema na waandishi wa habari walilazimika kusubiri kwa saa zaidi ya 12 kwenye kituo hicho cha kuhesabia kura hadi saa 12.50 alfajiri ya jana wakati Kagenzi alipotangaza matokeo hayo.

Usiku huo ulikuwa ni wa taabu kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kati ya saa 8.00 usiku na saa 12.00 alfajiri huku kukiwa na katizo la umeme kwa zaidi ya mara mbili hivyo kukatiza mara kadhaa mchakato wa kujumlisha kura.Mvua hiyo ni kubwa ya kwanza kunyesha katika Wilaya ya Meru tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo mdogo Machi 9, mwaka huu hadi juzi wakati kura zilipoanza kujumlisha.


Maandalizi ya jenereta ya dharura yaliyokuwa yamefanywa na ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi, yaliwezesha kazi hiyo kuendelea hadi mchakato mzima ulipokamilika, hivyo kuwezesha mshindi kutangazwa saa 12.54 jana alfajiri.

Masanduku ya kura na fomu za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura vilianza kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi saa 1.20 usiku wa juzi na ilipotimu saa 7.00 usiku jana, tayari kata zote zilikuwa zimewasilisha taarifa zake. Hata hivyo kasoro iliyojitokeza ni pale polisi walipolazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana wakishangilia ushindi kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo.

Kati ya saa 2.00 na saa 4.30 usiku, mabomu hayo ya machozi na ya vishindo yalirindima mfululizo katika eneo la Usa River na kusababisha maduka, migahawa na baa kufungwa mapema.

Baadhi ya wafuasi wa Chadema walikamatwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema walikuwa na mpango wa kwenda kuwawekea dhamana katika Kituo Kikuu cha Arusha mjini ambako waliwekwa mahabusu.

Habari zinasema katika tafrani hiyo, gari la Mkuu wa Operesheni ya Polisi katika Uchaguzi wa Igunga, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Issaya Mngulu lilivunjwa kioo chake baada ya kupigwa na jiwe kutoka kwa waandamanaji.

Hicho ni chanzo cha hasira za polisi ambao walirusha mabomu ya machozi kudhibiti hali hiyo maana tusingefanya hivyo hali ingekuwa mbaya zaidi,”alisema mmoja wa viongozi wa vikosi vya polisi ambaye hata hivyo hakutaka kutajwa gazetini.