Friday, March 30, 2012

WABUNGE KWENDA KUISHANGILIA SIMBA S.C ALGERIA


Mh Zitto Kabwe ataongoza kikosi cha wabunge kwenda Algeria kuipa Support Simba S.C

WABUNGE watano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamethibitisha kuambatana na Simba katika safari ya kuelekea Algeria tayari kwa kuivaa ES Setif katika pambano la marudiano lililopangwa kupigwa Aprili 6, nchini humo.

Pambano dhidi ya Waaarabu hao kutoka katika jiji la Setif nchini humo ni la marudiano baada ya pambano la awali lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuishuhudia Simba ikiondoka na ushindi wa 2-0.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage aliwataja wabunge hao kuwa ni pamoja na Zito Kabwe (Kigoma Kusini), Musa Hassani Zungu(Ilala), Asnein Murij, Murtaza Mangungu(Kilwa Kaskazini)na Khalifa Suleiman Khalifa(Gando).

Alisema kuwa wakati safari ya wabunge Mangungu, Murij na Khalifa itaanzia Dar es Salaam, Kambwe ataanzia safari yake ya kuelekea Algeria akitokea nchini Nigeria huku Zungu akitarajiwa kuungana nao akitokea nchini Morocco alikodai yupo kwa sasa.

Aliongeza kuwa mbali ya wabunge hao, mashabiki 18 wa klabu pia wamethibitisha kuwa watasafiri na kikosi cha timu yao kwa ajili ya kuwaunga mkono ikiwa ni baada ya kununua tiketi za ndege.

"Kimsingi maandalizi ya safari ya Algeria yanaendelea vizuri na hapa tunapoongea tayari wabunge watano akiwemo mheshimiwa Zitto, Zungu, Murij, Mangungu na Klalifa wamethibitisha kuungana nasi kule Algeria."

Kuhusu mapokezi pindi watakapotua nchini Algeria, Rage alisema mpaka wakati huu uongozi wake umekuwa ukiwasiliana mara kwa mara na wanafunzi wanaosoma nchini humo kwa ajili ya kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

"Hatuna ofisi ya ubalozi Algeria, lakini tunashukuru Wizara ya Mambo ya Nje inatupa msaada mkubwa, pia tuna mawasiliano na wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma kule ambapo tayari wamejipanga kutupokea na kutupa msaada utakaohitajikika,"alisema Rage