Friday, March 23, 2012

SIMBA YAAHIDI KUWAANGAMIZA WAARABU

Timu ya soka ya Simba imewatoa hofu Watanzania kwa kuahidi kuvunja mwiko wa kufungwa na Waarabu kwa lengo la kulinda heshima ya soka la Tanzania hapo Jumapili watakapocheza dhidi ya ES Setif katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Wito huo umetolewa na washambuliaji Emmanuel Okwi, Uhuru Selemani na nahodha Juma Kaseja jana kabla ya kuelekea kwenye mazoezi yao ya jioni jana walipozungumzia malengo yao katika mchezo huo, huku wakidai kuwa timu za Waarabu zimekuwa zikiwasumbua mara kwa mara.

Wachezaji hao walisema Watanzania wanatakiwa kuwaamini kwa kuwa wako kikamilifu na wamejipanga kuweka historia ya kweli katika pambano hilo linalosubiriwa na mashabiki kwa hamu.

"Tunahitaji ushindi wa mabao zaidi ya moja hapa ili kujiwekea mazingira mazuri katika mchezo wa marudiano tutakapokuwa ugenini."

"Utakuwa mchezo mgumu, kwani mara nyingi tunapokutana na hizi timu za Waarabu wamekuwa wakitufunga, lakini sasa tunataka kuvunja mwiko huo wa kufungwa kila mara na kuhakikisha tunashinda kwa magoli mengi,"alisema Uhuru.

Naye kinara wa ufungaji wa Simba, mshambuliaji Okwi aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuwashangilia kwa nguvu.

"Unajua kila mmoja anategemea ushindi na amejipanga kwa namna yake, tunawataka Watanzania watuombee ili tushinde na hatimaye tuiwakilishe nchi katika hatua nyingine ya mashindano haya," alisema Okwi kwa kujiamini.

Nahodha wa Simba, Kaseja alisema ushindi wa mapema ni muhimu kwao na watahakikisha wanatumia vyema kila nafasi wanayopata huku akiwataka wachezaji wote kuwa na ushirikiano wa kutosha miongoni mwao ambao utaongeza ari ya ushindi.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella 'Golden Boy' aliwataka wachezaji wa Simba kufuata maelekezo yote watakayoambiwa na kocha wao Cirkovic Milovan.

"Wakifuata maelekezo ya kocha watacheza kwa kujiamini na kutumia vizuri nafasi watakazopata, kwani hili ndio tatizo kubwa ninaloliona kwa wachezaji wa Tanzania hivi sasa,"alisema Mogella.

Katika mazoezi ya jana jioni kocha Milovan alitumia muda wake mwingi kuwafundisha mabeki wake namna ya kuokoa mipira ya kona, krosi na mipira ya juu.

Heshima ya soka ya Algeria

Vinara wa ligi ya Algeria, Setif wenyewe wamejipanga kwa ajili ya kujenga heshima ya soka ya nchi yao.

Kocha Alain Geiger wakati wote Setif inapocheza lengo lake la kwanza ni ushindi sio kitu kingine, ni kitu kilichoeleweka kwa wachezaji wake wote na hivyo wajibu wa wachezaji wake ni kuthibitisha ubora wao uwanjani.

Setif hawategemei kuingia uwanjani na kukaa nyuma kujilinda kwa kusubiri mashambulizi ya wapinzani wao kwa sababu silaha kubwa ya soka ya Algeria ni kushambulia kwa haraka.

Geiger anapendelea timu kujilinda kwa kukaa na mpira iwe kwa kushambulia kwa kasi au pasi fupi fupi na kwenda mbele kwa lengo ya kuichanganya ngome ya timu pinzani na kupata ushindi bila ya kuruhusu goli la kufungwa.

Mashabiki watulivu

Nyota wa Setif, Delhoum amesifia tabia ya ukarimu wa mashabiki wa Tanzania, kitu kinachotoa faraja kwao katika mchezo huo.

"Mashabiki wa Tanzania hawana matendo mabaya kwa timu za kigeni wanajulikana kwa utulivu wao na tabia yao nzuri ya uanamichezo," alisema Delhoum aliyecheza katika mechi kati ya Algeria dhidi Taifa Stars mwaka jana.