Monday, March 19, 2012

SIMBA S.C NI NOMAAAA YAILIZA MTIBWA 2-1


Siku ya jana ilikuwa mbaya kwa kiungo Patrick Mafisango jana alipiga penalti mara mbili akakosa, lakini bado Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Mafisango alikosa penalti hiyo iliyotokana na mshambuliaji Emmanuel Okwi kuchezewa rafu katika eneo la hatari katika dakika ya 59. Alipiga mara ya kwanza akakosa lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai ya kipa kuvuka mstari, hata hivyo alipopiga tena Deogratius Munishi ambaye ni kipa wa zamani wa Simba akadaka tena.
Katika mchezo huo, Simba walipata bao katika dakika ya 18 lililofungwa na Mafisango baada ya kuitumia vizuri krosi ya Okwi. Mtibwa Sugar walirejea kwa kasi katika kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 52 kupitia kwa Hussein Javu aliyepiga shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari.
Huku timu zote zikionekana kushambuliana kwa zamu, walikuwa ni Simba waliofanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani wao baada ya mshambuliaji mrefu, Felix Sunzu kufunga kwa kichwa akipokea mpira wa faulo iliyopigwa na Okwi.
Mtibwa ndiyo waliowahi kulisakama lango la Simba katika dakika ya tatu. Mshambuliaji wa timu hiyo, Javu alibaki yeye na mlinda mlango Juma Kaseja lakini akashindwa kuutumbukiza mpira wavuni.
Beki wa Simba, Mkenya, Derrick Walulya, jana alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi tangu asajiliwe na Wekundu wa Msimbazi, Januari, mwaka huu, ingawa alilaumiwa na wachezaji wenzake uwanjani kwa kuonekana kuwa uchochoro, alijitahidi kwa kiasi chake.
Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri huku akiuponda Uwanja wa Jamhuri kwamba hauna ubora, wakati Kocha wa Mtibwa, Tom Olaba alimshutumu mwamuzi kwa kushindwa kuchezesha vizuri pambano hilo.
Katika michezo mingine iliyopigwa jana, Azam iliifunga Ruvu Shooting kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, wakati Toto African ilifufua matumaini yake ya kubaki ligi kuu kwa kuibamiza Polisi kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

MAN UNITED KIBOKO,YAITENGENEZA WOLVES 5-0


Welbeck akishangilia goli

Manchester United imezidi kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu ya England na kuongeza wigo wa pointi nne dhidi ya Manchester City, baada ya kuilaza Wolves mabao 5-0.
Jonny Evans alikuwa wa kwanza kuipatia bao Manchester United, kabla mlinzi wa Wolves Ronald Zubar hajatolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya manjano.
Hali hiyo ilikuwa ni afueni kwa wageni ambapo Antonio Valencia alifunga bao la pili kabla ya Danny Welbeck kutumbukiza wavuni bao la tatu.
Man U 5-0 Wolves

Javier Hernandez baadae alipachika bao la nne kwa kuunganisha vyema mpira wa pembeni uliopigwa na Valencia na muda mfupi baadae Steven Fletcher nusura aipatie Wolves bao la kufutia machozi. Alikuwa Hernandez tena aliyeifungia Manchester United bao la tano.
Wolves sasa wameshinda mchezo mmoja tu kati ya michezo 14 iliyopita ya ligi na wanamuweka meneja wao wa muda Terry Connor katika wakati mgumu wakiwa mkiani mwa msimamo wa Ligi.
Hii ni mechi ya tatu Wolves kupoteza wakiwa chini ya Connor katika mechi nne alizosimamia na wameshafungwa mabao 12 katika mechi tatu na wao bila kutumbukiza mpira wavuni.
Kwa kikosi cha Sir Alex Ferguson ushindi huo umewaongezea hazina ya mabao na kupunguza wigo wa mabao dhidi ya Manchester City na sasa kuwa mabao matatu tu.

FABRICE MUAMBA MAHUTUTI BAADA YA KUANGUKA NA KUZIMIA KWENYE MECHI

Fabrice Muamba kabla ya  kuzirai uwanjani
Fabrice Muamba muda mfupi kabla hajaanguka na kuzirai

Kiungo wa Bolton, Fabrice Muamba, anakabiliwa na saa 24 muhimu sana za maisha yake, meneja wa Bolton Owen Coyle alisema.
Bado anatibiwa katika kitengo cha wagonjwa mahtuti.
Meneja wa Bolton Wanderers, Owen Coyle, alisema anatumai matokeo yatakuwa mema kwa Fabrice Muamba, huku mchezaji huyo anaendelea kuuguzwa.
Coyle alisema hayo nje ya London Chest Hospital, ambako ndiko Fabrice anakotibiwa baada ya kuzirai wakati Bolton Wanderers wanacheza na Tottenham Hotspur kwenye uwanja wa White Hart Lane saa 12 magharibi.
Imejulikana leo kuwa matabibu wasaidizi hawakuweza kuufanya moyo wa kijana huyo wa umri wa miaka 23, kuanza kupiga tena wenyewe kwa karibu saaa mbili, baada ya kubanwa na moyo.
Bolton Wanderers wakicheza na Tottenham Hotspur kwenye robo fainali ya kombe la FA.
Coyle aliwaambia waandishi wa habari: "Tunatumai atapona"
Muamba alizaliwa Zaire (sasa inajulikana Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na alifika England akiwa na umri wa miaka 11.
Mchezaji huyo kabla ya kujiunga na Bolton Wanderers alitokea klabu ya Birmingham mwaka 2008 na amecheza mechi 148 katika klabu yake ya sasa.
Mashabiki wa timu zote mbili walikuwa wakiimba jina la Muamba wakati alipokuwa akitolewa uwanjani kwa machela.
Na Muamba alikumbukwa katika mechi zote zilizochezwa Jumapili