Monday, March 12, 2012

Swansea yaipopoa Man City Kileleni, Man United yakalia usukani


Wayne Rooney akitupia kambani goli la kwanza la United dhidi ya WBA.

Manchester United imefanikiwa kukalia kiti cha Ligi ya Kuu ya England kwa mabao mawili yaliyopachikwa na Wayne Rooney na kuilaza West Brom.
United imepata nafasi hiyo ya kukalia kiti cha uongozi baada ya Manchester City kuteleza kwa kulazwa bao 1-0 na Swansea.
Rooney aliifungia Manchester United bao la kwanza kabla ya mapumziko, alipounganisha mpira uliopigwa na Javier Hernandez ambao ulimpita mlinda mlango Ben Foster.
Mshambuliaji huyo wa Manchester United alifunga tena bao la pili kwa mkwaju wa penalti, wakati mlinzi wa West Brom Jonas Olsson alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.
Man united 2-1 West Bromwich Albion

Wakiwa wamesaliwa na michezo 10 kabla ya msimu wa ligi kumalizika, Manchester United sasa wanapewa nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake baada ya Manchester City kuteleza.
Matumaini ya Manchester City kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England yaliingia dosari baada ya bao la kichwa dakika za mwisho la Luke Moore lilipoipatia Swansea ushindi wa bao 1-0.

Young na Rooney wakishangilia Goli

wansea City kwa ushindi huo sasa imeacha wazi mbio za kuwania ubingwa ligi ya England baada ya ushindi huo katika uwanja wao wa Liberty.
Kikosi cha Roberto Mancini kiliponea chupuchupu kufungwa dakika za mwanzo za mchezo wakati Joe Hart alipookoa mkwaju wa penalti wa Scott Sinclair baada ya Hart kumuangusha Wayne Routledge ndani ya sanduku la hatari.
Swansea ilipata bao lake hilo moja baada ya Moore kuunganisha kwa kichwa mpira wa pembeni wa Routledge zikiwa zimesalia dakika saba kabla mchezo kumalizika.
City hawakucheza vizuri ingawa Micah Richards dakika za mwisho alifunga bao ambalo lilikataliwa kwa vile alikuwa ameotea.
Manchester City sasa wanashikilia nafasi ya pili wakiwa na pointi 66 na Manchester United wamekusanya pointi 67.

Chelsea yazinduka usingizini,Liverpool yapokea kichapo kutoksa kwa Sunderland


Didier Drogba akiwa katika harakati za kufunga na kufanikiwa kuipatia goli Chelsea


Drogba akishangilia goli dhidi ya Stoke City nyuma ni Sturridge na Juan Mata
Chelsea 1-0 Stoke City

Didier Drogba umaliziaji wake maridadi umeihakikishia ushindi ingawa mwembamba Chelsea dhidi ya Stoke City iliyokuwa ikicheza pungufu ya mchezaji mmoja katika pambano la kwanza la Roberto di Matteo kusimamia akiwa meneja wa muda Chelsea katika Ligi Kuu ya England.
Stoke walicheza karibu mchezo wote wakiwa na wachezaji 10 baada ya Ricardo Fuller kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumtimba pajani Branislav Ivanovic.
Chelsea mipira yao iligonga mwamba mara mbili lakini iliwabidi wawe waangalifu kuikabili Stoke City iliyokuwa ikijihami vizuri.
Lakini Drogba hatimaye akamaliza kazi baada ya kumzunguka mlinda mlango Asmir Begovic baada ya kupokea pasi ya Juan Mata na kupachika bao lake la 100 tangu aanze kucheza Ligi Kuu ya England.
Hali ya kusua-sua kwa Liverpool kwenye ligi imeendelea tena baada ya kuchapwa na timu iliyoonesha ari ya kusaka ushindi ya Sunderland.
Baada ya kosakosa za kipindi cha kwanza, Sunderland walifanikiwa kuongoza kwa kupachika bao baada ya mkwaju wa Fraizer Campbell kuzuiwa na mlinda mlango Pepe Reina kabla ya Nicklas Bendtner kuuwahi na kuutumbukiza wavuni.
Liverpool waliwaingiza Steven Gerrard na Andy Carroll lakini mabadiliko hayo hayakuzaa matunda kwa upande wa wao.

Niclas Bendtner akishangilia goli alilofunga dhidi ya Liverpool

Sunderland 1-0 Liverpool

Sunderland walijihami vyema kulinda bao lao moja dhidi ya Liverpool ambao nusura wangesawazisha.
Junior Hoilett akifunga mabao mawili ameisaidia timu yake ya Blackburn kupanda juu kutoka eneo la hatari la kuteremka daraja na kuicha Wolves wakicheza uwanja wa nyumbani wakiendelea kusuasua eneo la kuteremka daraja wakiwa nafasi moja tu kutoka mkiani.
Mashabiki wa Wolves walifanya maandamano kabla ya mchezo dhidi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu yao ya Wolves Jez Moxey kwa kumteua Terry Connor kushikilia nafasi ya umeneja na hatimaye wakashuhudia timi yao ikiporomoka kwa kuonesha kiwango cha chini.
Hoilett alifunga bao lake la kwanza baada ya kumiliki mpira wa kimo cha mbuni na kuachia mkwaju kutoka upande wa kona na kuingia moja kwa moja wavuni.
Na baadae mshambuliaji huyo akafanikiwa kufunga bao lake la pili kwa mkwaju wa yadi 25 mara tu baada ya kuanza kipindi cha pili.
Kufungwa huko kumeicha Wolves nafasi ya 19, nafasi moja tu kutoka mkiani wakiwa wamepata ushindi wa mchezo mmoja tu katika mechi 14 za Ligi zilizopita.
Bao la kwanza la Andreas Weimann la Ligi Kuu ya England liliipatia ushindi Aston Villa dhidi ya Fulham waliokuwa wakicheza kwa kiwango cha juu na hatimaye wakamaliza kwa huzuni katika uwanja wa Villa Park.
Villa walimiliki mchezo katika kipindi cha kwanza huku Gabriel Agbonlahor nusura angepachika bao.
Marc Albrighton alipiga mkwaju uliogonga mwamba katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili na baadae Damien Duff wa Fulham mkwaju wake nao ukagongwa mwamba. Hadi mwisho Aston Villa 1 Fulham 0.
Meneja wa QPR Mark Hughes aliachwa asifahamu la kufanya baada ya kushuhudia timu yake ikinyimwa ushindi baada ya bao la dakika za mwisho la Ivan Klasnic kuipatia ushindi wa mabao 2-1 Bolton.
QPR ilitakiwa kuwa mbele kwa bao moja kipindi cha kwanza lakini mpira wa kichwa aliochonga Clint Hill haukuhesabiwa bao licha ya mpira kuonekana umevuka mstari.
Bolton iliongoza kwa bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Darren Pratley kabla Djibril Cisse kusawazisha kwa mkwaju wa karibu, ingawa baadae picha za televisheni zilizokuwa zikirudiwa zilionesha alikuwa ameotea.
Lakini bao la dakika za mwisho la Klasnic aliyepokea pasi murua kutoka kwa Ryo Miyaichi na kufanikiwa kumpita mlinda mlango Paddy Kenny, liliitoa Bolton kutoka eneo hatari la kuteremka daraja.