Thursday, February 16, 2012

ARSENAL NYANYA YASASAMBULIWA 4-0 NA AC MILAN

Robinho alikuwa mwiba mkali kwa Arsenal

Matumaini ya Arsenal kuvuka salama robo fainali za klabu bingwa Ulaya ni kitumbua kilichotiwa mchanga, baada ya Jumatano jioni kunyoroshwa magoli 4-0 na AC Milan ya Italia katika mechi ya mkondo wa kwanza, ikiwa ni kati ya timu 16 zilizosalia katika mashindano hayo.
The Gunners hawakuwa na lao tangu Kevin-Prince Boateng alipoiwezesha Milan kupata bao la kuongoza.
AC MILAN 4-0 ARSENAL

Mchezaji wa zamani wa Manchester City, Robinho, aliongezea bao la pili kwa kichwa, na kuongezea na la tatu, kuihakikishia timu yake ilikuwa na uhakika wa kupata ushindi.
Zlatan Ibrahimovic alikamilisha kibarua kwa kuandikisha bao la nne la penalti, na wakati huohuo akiandikisha historia kwa upande wa Arsenal, ikiwa ndio matokeo mabovu zaidi ya Arsenal kufungwa kwa mabao mengi kiasi hicho katika pambano la Ulaya.
Miaka minne iliyopita, Arsenal ilikuwa ni timu ya kwanza ya Uingereza kufanikiwa kuishinda AC Milan ikiwa nyumbani, katika uwanja wa San Siro, wakati ilipopata ushindi wa magoli 2-0 katika mechi ya mkondo wa pili, na kuiondoa timu hiyo kutoka vilabu 16 vilivyokuwa vimesalia katika mashindano hayo ya klabu bingwa.

Benchi la ufundi la Arsenal likiwa limelowa kwa kipigo cha 4-0

Arsenal ya wakati huo ilikuwa tofauti kabisa na timu iliyoshiriki katika mchezo wa Jumatano jioni.
Mwaka 2008 Arsenal ilikuwa na uhodari mkuwa wa ulinzi, na ilicheza kwa ustadi na ikawa ni burudani kwa mashabiki wengi, kinyume na Arsenal ilivyopambana katika mechi hiyo ya San Siro.
Mshambulizi Robin van Persie amekuwa ni nyota msimu huu, lakini katika uwanja wa San Siro, inaelekea alikuwa zaidi ni abiria, na mkwaju wake uliokuwa na matumaini katika kipindi cha pili ukizuiwa na Christian Abbiati, na hata nguvu mpya za Thierry Henry alipoingia uwanjani baadaye hazikubadilisha lolote.
Bila shaka akiwa katika ndege kuelekea New York, Henry atawaza ni kwa nini aliamua kuichezea tena Arsenal.

Mambo magumu, wachezaji wa Arsenal Thierry Henry,nahodha Van Persie,Song (17) na Djourou(20) wakijadili jambo kabla ya kuanza mpira baada ya goli la tatu.

Meneja wa Arsenal alikuwa na matumaini kwamba Henry angelibadilisha mambo alipoingia katika kipindi cha pili, lakini hata kabla ya kuupata mpira, Milan tayari walikuwa wameandikisha bao la tatu.
Wenger atawaza pia juu ya umuhimu wa kufuzu kushirikishwa katika mechi za klabu bingwa, halafu kupigwa mabao mengi kiasi hicho.