Friday, February 10, 2012

BIG UP TIMBULO WANAOSEMA NA WASEME


Timbulo

BIG UP TIMBULO,..Wale wote wanaosema Timbulo kakopi ule wimbo wa Domo langu kutoka kundi la Xmalea wa Ivory Coast nawapinga vikali, Timbulo amekiri aliipata hiyo ngoma kabla na akachukua idea tu na sio kukopi kama inavyosemwa mitaani.
Kwa kifupi nampongeza sana Timbulo hata kama idea ni ya mtu lakini ametumia ujuzi mwingi katika kutunga na kuimba mpaka song likatoka poa..wanaomsema na nyinyi jaribuni kukopi halafu mtoe song likubalike kama mnaona ni rahisi.

Song la Timbulo Domo langu

Nimesikiliza kipindi mtoto Adam Mchomvu anamponda Timbulo kwa kusema eti kakopi na kupesti, nadhani elimu Adam hana ya nini maana ya kukopi na kupesti. Kukopi na kupesti inamaana haubadilishi kitu unachukua kitu kama kilivyo toka sehemu moja na kukiweka sehemu nyingine bila kupunguza ama kuongeza kitu.
Katika song waliloimba hao wa Ivory Coast wameimba lugha tofauti na melody tofauti, Hapo utaona kazi kubwa ameifanya Timbulo ya kupata idea halafu akatafuta mashairi yake binafsi yakaendana na ile idea halafu akaimba kwa ustadi mpaka ikakubalika sio kazi ndogo kama unabisha jaribu wewe uone kama utapata kitu.
Ni kazi sana kuchukua idea ya mtu halafu ukatoa kitu kikakubalika kuliko kile kilichokupatia idea kuliko kutoa kitu chako binafsi, mara nyingi hata wasanii wa nje huwa wanajitahidi kutoa track kali na inapofikia kutoa remix wanahakikisha iwe kali kuliko track halisi, haina maana ukitoa track kali ikapendwa halafu ukatoa remix ikawa utumbo inakuwa haina maana.
Mwisho kabisa Adam na wenzako naomba niwape maana ya sanaa na msanii inawezekana hamjui ndio maana mnaropoka tu.

Sanaa ni upangaji wa dhana kulingana na hisia na mawazo ya msanii, na msanii ni mtu anaepanga dhana kulingana na hisia na mawazo yake.
Timbulo songa mbele wanaopiga kelele ni mashabiki wa muziki na sio wapenzi wa muziki kwani kuna tofauti kubwa kati ya mshabiki na mpenzi.
Big up Timbulo kama kukopi ni rahisi hakuna asietaka track yake iwe juu waambie na wao wakopi tuone.

PINDA anastahili kuwajibishwa


Waziri mkuu Mizengo Pinda

Madaktari wamerudi makazini baada ya kuafikiana na serikali kutoka katika mgomo uliodumu kwa takribani wiki mbili.
Sasa basi kama serikali ina uwezo wa kuwasikiliza madaktari na wakaafikiana warudi makazini kama alivyofanya waziri mkuu Mh Mizengo Kayanza Pinda, kwanini hawakuwasikiliza mapema na wakaafikiana kabla ya watanzania wasio na hatia kupoteza maisha yao kutokana na mgomo huo?
Ina maanisha serikali imefanya uzembe kwa kitu ambacho wana uwezo nacho,na uzembe huo umesababisha usumbufu,maumivu,gharama,hasara na VIFO vya watanzania walipa kodi walioiweka serikali hii madarakani, je ni nani anawajibika katika hili? nani atafidia gharama,muda,maumivu na VIFO vya watanzania wasio na hatia kutokana na mgomo huo wa madaktari uliodumu kwa takribani wiki mbili?
Kwa ukweli huu je? nitakuwa nina makosa kama nikisema Viongozi wote wenye dhamana katika serikali hii wawajibike kwa hili, nina maanisha kuanzia Rais wa nchi na "mnyororo" wote unaofuatia baada ya yeye.

Watanzania wenzangu nina uchungu mkubwa kutokana na vifo vya watu wasio na hatia kupoteza maisha kwa uzembe wa watu wachache tena ambao wapo kwa ridhaa ya wananchi walioteseka na waliopoteza maisha kutokana na uzembe wa serikali wa kutokuwasikiliza wananchi wanahitaji nini kwa wakati gani. Ni nani serikalini alikuwa hajui kuwa madaktari wanaandaa mgomo? bila shaka madaktari ni watu wasomi na makini sidhani kama walikurupuka tu asubuhi na kusema leo tunagoma bila sababu na bila taarifa, kama matatizo na sababu zao kugoma zilijulikana kwanini wakapuuzwa na wao kufikia hatua ya kugoma na kusababisha hasara,maumivu na VIFO vya watanzania walipa kodi wasio na hatia? wapo wanapaswa kuwajibika kuanzia kiongozi aliepokea taarifa hizo kama alitakiwa kuzifikisha kwa anaefuatia baada ya yeye na anaefuatia mpaka mwenye maamuzi ya mwisho wote hawa wanapaswa kuwajibika.

Naipinga kauli ya Waziri mkuu Mizengo Pinda alipotangaza kuwa serikali imeamua kuwasimamisha kazi naibu katibu mkuu Wizara ya afya na ustawi wa jamii mama Blandina Nyoni na mganga mkuu wa serikali Dk Deo Mtasiwa, na kusema kuwa swala la mawaziri kuwajibika ni la kisiasa. Hapa mkuu sijakuelewa kabisa swala la huduma na haki ya jamii wewe unasema ni la kisiasa? BIG NO, wanapaswa kuwajibika haraka sana.

Watanzania wenzangu hatutaonekana wakorofi au hatufai kama tukiishinikiza serikali kuwawajibisha wote waliopo katika utekelezaji wa madai ya madaktari kwa kuwa hakuna lolote linaloweza kulipa machungu ya wafiwa na maisha ya watanzania waliopoteza maisha pasipo hatia
MUNGU IBARIKI TANZANIA     MUNGU WABARIKI WATANZANIA HASA WALALAHOI

Al-Shabaab waungana rasmi na AL-Qaeda waapa kuiangamiza Marekani

Mkuu wa Al-Shabaab Ahmed Godane

Kundi la Waislam wenye itikadi kali nchini Somalia, al-Shabaab, limetangaza kuwa linaungana na kundi la al-Qaeda.
Tamko hilo limetolewa katika picha ya video iliyotolewa na makundi hayo mawili

Yusuf Garaad wa Idhaa ya Kisomali ya BBC ambaye ameitazama video hiyo amesema kundi hilo ambalo jina lake kamili ni Harakat al Mujahiddin al Shabaab, limetangaza rasmi kuungana na al-Qaeda.
Madai ya muungano huo yametolewa na kiongozi wa al-Shabaab, Ahmed Godane, au maarufu kama Abu Zubair.
Mkuu wa al-Qaeda, Ayman al-zawahiri

Akizungumza kwa lugha ya Kiarabu,Abu Zubair amesema sasa watatii maelekezo kutoka kwa kiongozi wa al-Qaeda, Ayman al-Zawahiri.
Akizungumzia Marekani, Ahmed Godane amesema wakati wa dola pekee duniani- Marekani - sasa umefikia mwisho na kuwa utawala wa Uislam ndio utachukua mamlaka.
Kiongozi wa al-Qaaeda, Ayman al-Zawahiri, ambaye pia ameonekana katika video hiyo, ameisifia al-Shabaab na kukiri na kukubali kwa kundi hilo kuungana na al-Qaeda.
Amesema hizo ni habari njema kwa wafuasi wake.

Wapiganaji

Al-Zawahiri amesema Somalia itakuwa ngome ya Jihad katika pembe ya Afrika na kuongeza kuwa watateketeza kile alichotaja kuwa ni kiburi cha majeshi ya Kikristo kutoka Marekani, Ethiopia na Kenya dhidi ya Wasomali.
Ametoa wito kwa al-Shabaab kulinda watu wake hasa wale ambao ni dhaifu, na pia kutaka kwa wananchi wa Somalia kuunga mkono uamuzi wa vijana wao, akimaanisha al-Shabaab.
Al-Shabaab ni kundi lenye wapiganaji maelfu kadhaa, wengi wao wakiwa ni Wasomali. Hata hivyo wanao pia wapiganaji wa kigeni kutoka katika nchi zinazoizunguka Somalia na hata sehemu nyingine duniani.
Mitindo yao ya upiganaji ni pamoja na mabomu ya kujitoa mhanga na pia ya kutegwa ndani ya magari.

Mwenendo

Al-Shabaab kwa sasa inadhibiti maeneo kadhaa ya kusini na kati ya Somalia.
Katika miezi kadhaa iliyopita wamekuwa wakibanwa kutoka pande kadhaa. Mjini Mogadishu wanapambana na majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika, Amisom, yenye wanajeshi kutoka Uganda, Burundi na Djibouti. Majeshi hayo yanadhibiti zaidi mji mkuu, Mogadishu.
Upande wa kusini, majeshi ya Kenya yameshambulia ngome za al-Shabaab ardhini, baharini na angani. Majeshi ya Ethiopia pia yanashambulia kundi hilo kwa upande wa kaskazini na tayari wameteka mji wa Beled Weyne, mji muhimu katikati mwa Somalia.
Kuungana kwa al-Shabaab na al-Qaeda huenda kukabadili mwenendo mzima wa mzozo wa Somalia.