Thursday, February 2, 2012

VALENCIA 1-1 BARCELONA

SIMBA YAENDELEZA DOZI YAIKANDAMIZA JKT OLJORO 2-0
















Uhuru Selemani wa Simba akifanya vitu vyake

JKT Oljoro jana walishindwa kwenda sambamba na kasi ya Simba waliocheza pungufu sehemu kubwa ya mchezo na kukubali kipigo cha mabao 2-0, shukrani kwa mabao ya kipindi cha pili ya mshambualiaji, Emmanuel Okwi yaliyoihakikishia Wekundu hao wa Msimbazi pointi zote tatu.
Katika mechi hiyo iliyochangamshwa na ushindani mkubwa toka timu zote mbili kwenye Uwanja wa Taifa, ilishuhudia kiungo wa Simba Haruna Moshi 'Boban' akionyeshwa kadi nyekundu isiyo na onyo baada ya kumrushia teke la makusudi mchezaji wa Oljoro, Omary Mtaki dakika ya 42.
Mwamuzi Isiaka Shirikisho wa Tanga, ambaye alionekana kushindwa kwenda sawa na kasi ya mchezo, pia aliwalima kadi za njano Omary Khasim wa JKT kwa kumchezea vibaya Haruna Moshi, kisha Kelvin Yondani na Jonas Gerald wa Simba kwa kuwachezea vibaya Kalege Mgunda na Nyambele.
Ushindi huo umeifanya Simba kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo kwa kufikisha pointi 34, tatu mbele ya mahasimu wao Yanga watakaoshuka dimbani mwishoni mwa wiki hii.
Katika mechi hiyo ambayo Simba walitumia zaidi viungo kufanya mashambulizi, JKT Oljoro waliofungwa 2-0 mzunguko wa kwanza, itabidi wajilaumu kwa kushindwa kutumia ya fursa ya wapinzani wao kucheza pungufu kupata ushindi.
Kocha wa Oljoro, Ally Kidy mara baada ya mchezo alikiri kuzidiwa na Simba, lakini akawalaumu wachezaji wake kushindwa kutumia vizuri nafasi nyingi za kufunga walizopata na pia kutumia mwanya wa Simba kucheza pungufu.
Simba walitawala dakika 20 za mwanzo wa mchezo na kukosa mabao kadhaa, huku Oljoro wakirejea mchezo dakika 10 za mwisho za kipindi hicho baada ya awali kufunikwa sehemu ya kiungo.
Mabadiliko yaliyofanywa na Simba kumtoa Gervais Kago na kuingia mshambualiaji wa kimataifa kutoka Uganda, Okwi katika kipindi cha pili ndiyo yaliyoipa ushindi timu hiyo.

Okwi, ambaye pengo la kutokuwapo kwake katika mchezo wa kwanza lilionekana wazi, alitumia dakika 15 tangu aingie uwanjani kuipeleka Simba mbele kwa bao zuri akimalizia pasi ya Uhuru Selemani.
Dakika nne baada ya bao hilo, Oljoro walikuja juu na kufanya shambulizi la nguvu ambalo nusura lizae bao la kusawazisha kufuatia piga nikupige kabla ya mabeki wa Simba kuokoa hatari.
Mchezaji Bakari Kigodeko wa Oljoro hatasahau nafasi ya wazi kufunga akiwa amebaki na nyavu na kisha kupiga mpira nje katika dakika ya 71.
Walikuwa Simba waliotawala mchezo bila kuonekana kama walikuwa pungufu uwanjani na kujipatia bao la pili dakika saba kabla ya filimbi ya mwisho baada ya Okwi kuinasa pasi ya Mafisango na kufunga bao hilo.
Kocha wa Simba Cirkovic Milovan aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha mchezo mzuri na kushinda mchezo huo pamoja na kwamba walicheza pungufu. "Matokeo mazuri kwetu, ni ishara ya kuwa tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Kiyovu ya Rwanda," alisema.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa Mbagala, nje kidogo ya jiji kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi kati ya African Lyon iliichapa Polisi Dodoma mabao 2-0.Mechi hiyo ilishuhudia timu zote zikishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza, huku Lyon wakionekana kufika zaidi langoni mwa wapinzani wao.
Wakicheza kwa kushambuliana, Semy Kessy aliifungia Lyon bao la kwanza dakika ya 30 kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Polisi, Gerald Mwingira baada ya awali kuwalamba chenga mabeki wa timu hiyo.Lyon walijihakikishia pointi tatu ushindi kwa kufunga bao la pili kupitia Sunday Juma baada ya kushirikiana vizuri na Samuel Ngasa katika dakika ya 76.

Mwenyeji Guinea atupwa nje kombe la mataifa ya Afrika,Botswana nayo yaangukia pua

Ghana ilijitengea nafasi yake katika robo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kutoka sare 1-1 na Guinea katika uwanja wa Franceville.
Black Stars
Ghana wametinga fainali baada ya kuongoza kundi D
Guinea walijitahidi kupata bao la ushindi, lakini hawakufanikiwa.
Ushindi wa Mali wa magoli 2-1 dhidi ya Botswana ulimaanisha Guinea wanaondoka pasipo kucheza robo fainali.
Ghana vs Guinea

Mechi kati ya Mali na Botswana ilichezewa mjini Libreville.
Botswana ilikuwa ya kwanza kufunga kupitia Mogakolodi Ngele, bao la ufundi mkubwa, na ambalo kipa Oumar Sissoka hakujui ni nini kimepita hadi wavuni.
Garra Dembele aliweza kuisawazishia Mali, kabla kiungo cha kati Seydou Keita kumaliza kazi kwa bao la ushindi.
Ushindi huo ulimaanisha kwamba Mali ilimaliza katika nafasi ya pili katika kundi D, nyuma ya Ghana.
Timu zitapumzika siku mbili, kabla mapambano mawili ya kwanza ya robo fainali kuchezwa siku ya Jumamosi.
Mali vs Botswana

74 WAFARIKI UWANJANI KATIKA VURUGU ZA SOKA MISRI


Moto ukiwaka uwanjani

Watu 74 wamefariki kufuatia ghasia kati ya mashabiki wa timu mbili katika mji wa Port Said, nchini Misri.
Taarifa hizo ni kwa mujibu wa televisheni ya taifa.

Mashabiki wakiwa wamevamia uwanja katika vurugu hizo

Watu hao walikiufa baada ya mashabiki kuanza kuingia uwanjani, baada ya mechi kati ya vilabu viwili vikuu vinavyoongoza ligi nchini humo, Masry na Al-Ahly, siku ya Jumatano.
Inahofiwa kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka, kwani zaidi ya watu 156 wamejeruhiwa.
Huu ndio msiba mkubwa zaidi nchini Misri kuwahi kutokea katika uwanja wa kandanda, alielezea naibu waziri wa afya nchini Misri.
“Huu ni msiba wa kusikitisha mno”, alisema Hesham Sheiha kupitia matangazo ya televisheni.
Kati ya waliokufa ni pamoja na maafisa wa usalama.

Wachezaji wakikimbia kunusuru maisha yao

Mwandishi wa BBC anaelezea kwamba ukosefu wa usalama mkali ambao hudumishwa kwa kawaida huenda ikawa ni jambo ambalo lilichangia kutokea ghasia hizo.
Polisi nchini Misri wametulia mno tangu kufanyika maandamano yaliyomtoa Rais Hosni Mubarak madarakani.

Kimenukaaaaaa

Katika mechi hiyo ya Jumatano, timu ya Port Said, Masry, ilipata ushindi wa magoli 3-1.
Walioshuhudia walielezea kwamba kulikuwa na hali ya wasiwasi muda wote wa mechi hiyo, tangu shabiki mmoja wa Al-Ahly alipoinua bango ambalo inadaiwa lilikuwa linawatukana mashabiki wa timu ya nyumbani.
Katika mitandao ya jamii, licha ya kutokuwepo ushahidi, uvumi umekuwa ukienea kwamba maafisa wa usalama walikuwa wanapanga njama ya kupambana na mashabiki wa Al-Ahly.
Maafisa wachache wa polisi walijitahidi kuwapa ulinzi wachezaji, lakini hawakufanikiwa kabisa.
Sehemu moja ya uwanja ilichomwa moto.
Maafisa wanaohusika wameelezea kwamba vifo vingi vilitokana na watu kupata majeraha makubwa ya kichwa kwa kupigwa au kukatwa, na wengine kuzimia hadi kufa wakati wa mkanyagano.
Ndege za helikopta zilitumwa hadi Port Said kuwasafirisha hadi hospitali mashabiki waliojeruhiwa.

Maiti zilizopoteza maisha papohapo

"Huu si mpira. Hivi ni vita na watu wanakufa mbele yetu", alisema mchezaji wa Al-Ahly, Mohamed Abo Treika.
Mbunge wa Port Said, Albadry Farghali, aliwalaumu maafisa wa usalama.
"Walikuwa wapi haya yote yakitokea?"
"Watu wa Mubarak bado wako uongozini. Kiongozi wa utawala ameng'atuliwa, lakini watu wake bado wapo madarakani", alielezea kupitia televisheni.
"Usalama uko wapi? Serikali iko wapi?"
Mjini Cairo, mwamuzi alisitisha mechi nyingine, alipoarifiwa juu ya ghasia za Port Said.
Jambo ambalo liliwafanya mashabiki kuchoma moto sehemu fulani za uwanja.
Mechi zote za ligi kuu zimefutiliwa mbali, na bunge jipya la Misri siku ya Alhamisi litakutana katika kikao cha dharura kuujadili msiba huu.