Monday, November 21, 2011

MAN CITY YAPAA,ARSENAL YAPETA

Manchester City ilipata mabao mawili kwa njia ya mikwaju ya penati wakati walipopata ushindi murua wa mabao 3-1 dhidi ya Newcastle.

Mlinzi Ryan Taylor aliunawa mpira eneo la hatari na kusababisha Manchester City kupata bao lao la kwanza kwa mkwaju wa penalti uliojazwa kimiani na Mario Balotelli. Sergio Aguero baadae akatengeneza pasi murua kwa mlinzi Micah Richards aliyemaliza kazi kwa kufunga bao la pili.
Richards aliangushwa na Hatem Ben Arfa ndani ya eneo la hatari na kusababisha Manchester City wapate bao la tatu na penalti hiyo ilifungwa na Aguero.
Hata hivyo wakijitahidi dakika za mwisho Newcastle walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi lililopachikwa na Dan Gosling baada ya kuuwahi mpira ambao ulipigwa na Demba Ba na kumgonga mlinda mlango Joe Hart.
Huo unakuwa mchezo wa kwanza kwa Newcastle kupoteza msimu huu.
Bao la dakika za mwisho lililofungwa na Leighton Baines kwa mkwaju wa penalti, liliipatia Everton ushindi wake wa pili wa ligi nyumbani msimu huu baada ya kuilaza Wolves mabao 2-1.
Stephen Hunt ndiye alikuwa wa kwanza kuipatia Wolves bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti baada ya kiungo Marouane Fellaini kumchezea rafu David Edwards ndani ya eneo la hatari.
Phil Jagielka aliisawazishia Everton baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa free-kick uliochongwa na Baines kutokea upande wa kushoto.
Alikuwa Baines aliyeipatia bao la ushindi Everton zikiwa zimesalia dakika saba kabla mchezo kumalizika kwa mkwaju wa penalti baada ya Stephen Ward kumsukuma Louis Saha ndani ya sanduku.
Queens Park Rangers ikiwa imeanza kufungwa na Stoke, ilibadilika na kuweza kushinda kwa mabao 3-2 ambapo walisawazisha kwa bao la Heidar Helguson.
Stoke wakicheza uwanja wa nyumbani walipata bao la kuongoza lililowekwa wavuni na Jon Walters aliyeachia mkwaju mkali wa pembeni, kabla ya Helguson kusawazisha kwa kichwa akiwa hajakabwa na mchezaji yeyote.
Luke Young aliipatia QPR bao la pili kabla ya Helguson kuongeza la tatu kwa mkwaju wa karibu na lango.
Ryan Shawcross alifanikiwa kuipatia Stoke bao la pili naye kwa mkwaju wa karibu, lakini dakika nazo zilikuwa zimewatupa mkono na QPR ndio waliondoka na washindi.
Shane Long amerejea kwa kishindo katika klabu yake ya West Brom na kuinyanyua timu yake hadi nafasi ya 10 na kuzidi kuiongezea matatizo Bolton baada ya kufunga bao la pili la ushindi.
Mshambuliaji huyo alifunga bao lake la nne kwa msimu huu wa ligi katika dakika ya 56 ikiwa ni wiki nne tu tangu alipoumia goti.
West Brom ndio walikuwa wa kwanza kupata bao lililopachikwa na Jerome Thomas alipotegua mtego wa kuotea na akamzunguka mlinda mlango Jussi Jaaskelainen.
Ivan Klasnic alisawazisha dakika chache baadae kwa mkwaju wa penalti baada ya Fabrice Muamba kufanyiwa rafu, lakini hadi mwisho West Brom 2 Bolton 1.
Yakubu alikuwa shujaa wa Blackburn baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 99 na kuipatia timu yake iliyokuwa ikicheza pungufu ya mchezaji mmoja sare ya mabao 3-3 dhidi ya Wigan.
Mshambuliaji huyo alisawazisha baada ya Wigan kuwa mbele kwa mabao 3-2.
Robin van Persie alikuwa mwiba wa kuotea mbali baada ya kuipatia timu yake ya Arsenal mabao 2-1 dhidi ya Norwich na timu hiyo kupata ushindi wake wa 10 kati ya mechi 12.
Van Persie akicheza kwa kiwango cha juu msimu huu, kwa mara nyingine alisaidia Arsenal kuweza kuamka na kuvuna pointi tatu ugenini.
Alipata bao lake la kwanza baada ya kuunganisha pasi ya pembeni kutoka kwa Theo Walcott na bao lake la pili lilitokana na pasi maridadi ya Alex Song.
Norwich walikuwa wa kwanza kuistua Arsenal walipofunga bao la kwanza lililofungwa na Steve Morison kutokana na makosa ya mlinzi wa Arsenal Per Mertesacker.

CHELSEA HOI MBELE YA LIVERPOOL,YALALA 2-1 NYUMBANI

Glen Johnson amefanikiwa kuipatia ushindi Liverpool kwa bao la dakika za mwisho wakati Chelsea ilipolala kwa mabao mabao 2-1 katika uwanja wao wa Stamford Bridge.
Liverpool yailaza Chelsea mabao 2-1
Steven Gerrad akishangilia bao

Liverpool walikuwa wa kwanza kupata bao katika kipindi cha kwanza lililofungwa na Maxi Rodriguez katika dakika ya 33 baada ya gonga ya hapa na pale ya Craig Bellamy na Luis Suarez.
Daniel Sturridge aliyeingia kipindi cha pili aliisawazishia Chelsea kutokana na juhudi kubwa iliyooneshwa na Florent Malouda katika dakika ya 55.
Branislav Ivanovic nusura aipatie Chelsea bao la pili alipopiga kichwa lakini mpira huo ukaokolewa, lakini alikuwa mlinzi wa upande wa kulia Johnson aliyeihakikishia pointi tatu muhimu Liverpoo kutokana na jitahada zake binafsi alipokokota mpira upande wa kushoto na kuwapita walinzi wa Chelsea kama anafanya mazoezi na kupachika bao safi la pili.

Misri "kimenuka" Zaidi wafariki katika maandamano


Waandamanaji wakiwa wamekusanyika katika uwanja wa Tahrir 18/11/2011

Mamia ya waandamanaji nchini Misri wameivamia tena medani ya Tahrir katika mji mkuu wa Cairo hata baada ya polisi na wanajeshi kutumia nguvu kuwaondoa.

Chini ya muda wa saa moja baada ya kuondolewa Tahrir,waandamanaji walirudi tena mahali hapo huku wakitoa matamshi dhidi ya utawala wa kijeshi wa Misri.

Katika makabiliano hayo mengine ya siku ya Jumapili, watu 11 wameripotiwa kuuwawa.Kutokana na vifo hivyo jumla ya idadi ya watu waliouwawa tangu siku ya Jumamosi imefikia 13.

Kwa mujibu wa madaktari watu wengine wapatao 900 wamejeruhiwa wakiwemo maafisa wa usalama 40.

Awali, waandamanji walilazimika kutoroka baada ya maafisa wa usalama kuwarushia gesi ya kutoa machozi na kisha kuwapiga kwa marungu.

Machafuko mengine pia yalishuhudiwa katika miji mingine ikiwemo , Alexandria, Suez na mji wa Aswan.


Waandamanaji wa chama cha Muslim Brotherhood na vyama vingine vinashiriki katika maandamano hayo

Wandamanaji hao ambao walikuwa wameziba nyuso zao ili gesi ya kutoa machozi isiwadhuru wanalalamika kuwa watawala wa kijeshi walikuwa na njama za kunyakuwa uongozi wa nchi hiyo.

Machafuko hayo yametokea kukiwa kumesalia wiki moja tu kabla ya uchaguzi wa maeneo bunge kuanza ambao utakuwa wa kwanza tangu Rais Hosni Mubarak kupinduliwa mwezi wa Februari.

Mwandishi wa BBC Helena Merriman amesema kuwa hali sio nzuri sana kwa sababu mara kunashuhudiwa hali ya utulivu na baadaye tena hali inabadilika na kuwa ya taharuki na watu kuanza kukimbia.

Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita makundi wa Kiiislamu pamoja na wakereketwa wengine wamekuwa wakifanya maandamano nchini Misri huku waandamanaji wakidai kuwa kuna njama za kubadilisha katiba ili kuruhusu baraza la kijeshi kuendelea kuwa na uwezo mkubwa.