Saturday, October 29, 2011

SIMBA NA YANGA LEO HATUMWI MTOTO GENGENI NI VUTA NIKUVUTE TAIFA













Patashika ya ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, leo kwa mara ya kwanza tangu kuanza msimu inafikia hatua tamu kwa mechi ya mahasimu wa jadi Yanga na Simba kuvaana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Miamba hiyo, Yanga mabingwa watetezi, na Simba vinara wa msimamo, wanakutaka katika mechi yao kwanza msimu huu, lakini ikiwa ni ya tano kwa mwaka huu pekee.

Zilikutana, mwanzoni mwa mwaka huu Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi, zikakutana tena Ligi Kuu-raundi ya pili, zikashuka tena dimbani fainali ya Kombe la Kagame, na kumaliza kwenye mechi ya Ngao ya Hisani.

Simba imeshinda (2-0) mara mbili, fainali ya Mapinduzi na Ngao ya Jamii lakini Yanga ikashinda fainali ya Kombe la Kagame bao 1-0, na kwenda sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu.

Dakika 90 za mwamuzi Oden Mbaga atakayesimama kati 'kuzihukumu' timu hizo zitatosha kuhitimisha, majigambo, mbwembwe, sifa na visasi vya kishabiki vilivyopendezesha jiji karibu wiki nzima sasa.

Yanga inashuka dimbani ikiwa bado na upya wa mabadiliko ya kocha waliyofanya siku chake kabla ya pambano la leo, ikiwa ni mara ya pili wanabadilisha kocha ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Pamoja na kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa Ligi Kuu kutoka mikononi mwa Simba, na Kombe la Kagame kwa kuifunga Simba, iliamua kumtema kocha Mganda, Sam Timbe na kumrejesha Kostadin Papic.

Papic atakuwa na jukumu kubwa la kupoza 'mgawanyiko' wa uteuzi wake kama kocha mpya kwa kuifunga Simba na kurejesha matumaini ya kutetea ubingwa.

Kwa upande wao Simba wanajivunia rekodi nzuri tangu kuanza kwa msimu, na mpaka sasa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo na inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Yanga.

Safu ya Simba itakayoongozwa na Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Haruna Moshi, itakuwa na jukumu zito kuipenya ngome ya Yanga itakayokuwa chini ya Nadir Haroub 'Cannavarro' na Shadrack Nsajigwa.

Nayo ngome ya Simba itakayokuwa chini ya Juma Nyosso, Victor Costa, Said Cholo na Juma Jabu itakuwa na kazi ya kuwazuia Kenneth Asamoah na Hamis Kiiza pamoja na Shamte Ali.

Kocha wa Simba, Moses Basena, alisema jana kwenye kambi ya timu hiyo, Bamba Beach, Kigamboni kuwa kikosi chake kiko kamili kwa mchezo huo, na kueleza wazi kuwa amejiandaa kushinda.

Kwa tathmini yake binafsi anasema Simba ndiyo iliyo bora kwa sasa kulinganisha na wapinzani wao, jambo ambalo kwa upande wa kocha Papic yeye anamini matokeo ni baada ya dakika 90.

Papic atawategemea pia Jerry Tegeta na Davis Mwape katika kulitia misukosuko lango la wapinzani wao.

Mbali na mwamuzi Mbaga ambaye amelalamikiwa na Yanga na Simba kuchezesha mechi hiyo akisaidiwa na Hamis Chang'walu na Mohamed Kanyenye wakati mwamuzi wa mezani ni Soud Abdi wa Arusha huku kamishna wa mechi akiwa Mohamed Nyange.