Tuesday, September 27, 2011

Oljoro yawachakaza walioidindia Simba yawalamba Toto 2-0

JKT Oljoro iliyopanda daraja msimu huu imetafuna mfupa uliowashinda Simba baada ya kuinyuka Toto African mabao 2-0 kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Pia jana Azam F.C ilishindwa kuendeleza kazi yake ya ushindi baada ya kulazimishwa suluhu na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi wakati kwenye uwanja wa Chamazi, JKT Ruvu vilevile waligawana pointi na Villa Squad.

Timu za Kanda ya Ziwa zilijijengea jina wiki iliyopita baada ya kutibua rekodi ya Simba, ambapo Kagera Sugar ilitoka sare ya 1-1 na na timu hiyo halafu Toto African ikatoka nayo sare ya 3-3 na vinara hao wa ligi, lakini mambo yamekuwa tofauti baada ya timu hizo mbili zote kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa vijana wa Arusha.

Iliwachukua dakika sita Oljoro JKT kupata bao la kuongoza kupitia Sunday Mussa aliyepokea pasi nzuri kutoka kwa Paul Nonga na kupiga shuti lililojaa wavuni.

Wakati Toto wakiwa hawaamini kinachotokea Oljoro waliandika bao la pili dakika ya 18 kupitia Amir Hamadi akiunganisha kwa kichwa krosi nzuri ya Nonga iliyomshinda kipa wa Toto, Mustapha Mabrouk aliyekuwa ametoka nje kidodo ya goli lake.

Mzuka wa mechi dhidi ya Simba haukuwa kwa Toto kwani nyota wao Mnigeria Darlington Enyima alikosa bao dakika 38 baada ya kupiga shuti nje akiwa yeye na kipa wa Oljoro.

Katika dakika ya 43 Castol Mumbala alitoa pasi mbaya kwa kipa wake ambaye alishindwa kutuliza mpira huo kwa mguu na kuamua kuudaka hivyo mwamuzi kumzawadia kadi ya njano Mustapha Mabrouk kwa kitendo hicho.

Kwa ushindi waliopata Oljoro wanasogea hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi 13 katika michezo nane, lakini ndoto ya timu ya Azam ya kuisogelea Simba kileleni ilififia baada ya kulazimishwa suluhu na Ruvu Shooting katika mechi ya ligi.

Mshambuliaji John Boko wa Azam alikosa bao katika dakika ya 32 baada ya kushindwa kumalizia kwa umakini krosi ya Ibrahim Mwaipopo.

Shooting walijibu mapigo kupitia Abdallah Juma aliyekosa bao katika dakika ya 62 baada ya kuwatoka mabeki wa Azam na kupiga shuti lililopanguliwa na kipa Mwadini Ally na kutoka nje.

Mshambuliaji John Boko alifunga bao katika mechi hiyo, lakini mwamuzi alilikataa hivyo kocha wa Azam, Stewart Hall alilalamikia bao hilo, lakini mwamuzi alisema mfungaji ameotea na kuahidi kupeleka picha ya video ya tukio hilo TFF kama uthibitisho.

Katika mechi hiyo wahudumu wa huduma ya kwanza wa Redcross walikuwa hawajavaa sare zao za kazi walipokuwa wakiingia uwanjani kuwahudumia wachezaji katika mechi hiyo ya Azam dhidi ya Ruvu Shooting.

Pia mashabiki waliojitokeza kwenye uwanja wa Mabatini kushuhudia pambano hilo walilalamikia uchache wa tiketi uliowafanya washindwe kuingia uwanjani hapo ili kushuhudia mchezo huo.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika kocha wa Shooting, Boniface Mkwasa alisema mchezo ulikuwa mgumu, lakini amewasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa moyo na kupata matokeo hayo mazuri na sasa wanajipanga kuikabili Mtibwa Sugar.

Wakati Mkwasa akisifu kiwango cha wachezaji wake hali ilikuwa tofauti kwenye Uwanja wa Chamazi kwani kocha wa JKT Ruvu, Charles Kilinda aliwalaumu wachezaji wake kwa kushindwa kucheza kama kawaida yao na kusababisha timu hiyo kupoteza pointi kwenye mchezo huo.

"Sijawahi kuona timu yangu ikicheza mpira mbovu kama waliocheza leo tangu nilipoanza kuifundisha miaka minne iliyopita,"alisema Kilinda.

Kilinda aliongeza labda wamechoka kwa sababu wapo wachezaji wachache kwenye kikosi chake kwa sababu wengine wamekwenda kwenye kozi za kijeshi.

Hata hivyo timu ya JKT Ruvu watajilaumu wenyewe kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga kupitia washambuliaji wake Hussein Bunu, Rajab Chau na Emmanuel Linjechele katika dakika ya 20, 32, 38 na 40 kwa mashuti yao kutoka nje.

JKT Ruvu wanaosifika kwa kucheza soka ya pasi nyingi na kuvutia walishindwa kuonyesha mchezo wao huo mbele ya Villa Squad na kushuhudia timu hizo zikienda mapumziko zikiwa hazijafungana.

Ruvu walimtoa Alhaji Zege na kumwingiza Haruna Adolf wakati Villa walimpumzisha Mohamed Kijuso na nafasi yake kuchukuliwa na Allu Bilal.

Katika mchezo huo makipa wa timu zote mbili Mohamed Bambino wa Villa Squad na Hamis Nyangalio wa JKT Ruvu walifanya kazi kubwa kulinda magoli yao.

SIMBA, MTIBWA ZAINGIZA Sh 74 mil

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Mtibwa Sugar iliyochezwa Septemba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh 74,345,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 13,285 ambapo kiingilio kilikuwa sh 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh 7,000 rangi ya chungwa, sh 15,000 kwa VIP C na B na sh 20,000 kwa VIP A.

Eneo lililoingiza watazamaji wengi ni kwenye viti vya bluu na kijani ambapo waliingia mashabiki 11,798 wakati eneo lililoingiza watazamaji wachache ni la VIP A ambapo waliingia mashabiki 58.

Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo ambazo ni sh 11,637,000 na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh 11,340,762.70 kila timu ilipata
sh 15,410,171.19.
Mgawo mwingine ulikwenda kwa gharama za mchezo (sh 5,136,723.73), uwanja (sh 5,136,723.73), TFF (sh 5,136,723.73), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh 2,568,361.86), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh 2,054,689.49) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh 513,672.37).