Thursday, September 22, 2011

Barcelona Valencia nguvu sawa 2-2

Timu ya Valencia ilifanikiwa kutoka sare na Barcelona katika mechi ya Ligi ya Spain inayoendelea nchini humo. Magoli ya Valencia yalifungwa na Abidal dk 12 aikijifunga na Hernandez dk 23 wakati ya Barcelona yalifungwa na Pedro dk 14 na la pili Fabregas dk 77.

Yanga,Azam mbele kwa mbele Simba yatoa sare na Toto Africans















Asamoah akijaribu kuwatoka walinzi wa Villa

Timu ya soka ya Yanga wamewanyuka Villa Squad wakiwa pungufu kwa "bakora" 3-2 kwenye Uwanja wa Chamazi huku vinara wa ligi Simba wakilazimisha sare ya 3-3 na Toto African jijini Mwanza.Wakati Yanga wakipata ushindi wao wa pili na kufikisha pointi tisa, matajiri wa Chamazi, Azam wenyewe wamesogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo kwa kufikisha pointi 14 na kuisogelea Simba inayoongoza kwa pointi 15 baada ya kupata sare ya tatu katika mechi saba.

Macho ya wengi yalikuwa Uwanja wa Chamazi, ambapo Yanga ilipokuwa na kibarua kizito mbele Villa Squad waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia Nsa Job, lakini mabingwa hao walisawazisha kupitia Haruna Niyonzima na Kenneth Asamoah na Hamis Kiiza waliongeza mabao mengine kabla ya Kigi Luseke kuifungia Villa bao la pili na kufanya matokeo kuwa 3-2.

Azam wenyewe wakiwa ugenini itabidi wamshukuru John Boko kwa kuwafungia bao pekee katika mechi dhidi ya Coastal Union akimalizia penalti yake iliyotemwa na kipa.

Katika mechi ya Yanga dhidi ya Villa, nyota wa kimataifa wa Yanga walilipa fadhila kwa kufunga mabao na kumpunguzia presha kocha wao Sam Timbe aliyepewa mechi tatu za kuhakikisha anapata ushindi.

Mshambuliaji Mwape alikosa bao katika dakika ya tano kwa kushindwa kuunganisha krosi ya Ally Shamte iliyotoka sentimita chache kutoka goli la Villa Squad.

Kenneth Asamoah naye alikosa bao baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Oscar Joshua na kutoka nje, wakati nyota hao wa Yanga wakikosa Nsa Job alitumia vizuri mwanya wa kipa Yaw Berko kutoka kwenye mstali na kuinua mpira juu na kujaa wavuni katika dakika ya 11.

Dakika nne baadaye Niyonzima aliisawazishia Yanga bao kwa mpira wa adhabu ambao aliupiga na kwenda moja kwa moja wavuni na kufanya matokeo kuwa 1-1.Kocha wa Villa Squad, Said Chamosi alimtoa Haruna Shamte katika dakika ya 24 na kumwingiza Evalist Maganga.

Kocha wa Yanga, Sam Timbe alimwaanzisha kwa mara ya kwanza Idrisa Rashid akicheza na Asamoah katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.Matunda ya Rashid yalionekana baada ya mchezaji huyo kupitisha krosi nzuri kwa Asamoah aliyefunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ya Tanzania na kuifanya Yanga kuongoza mabao 2-1 katika dakika ya 27.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ghana alipoteza nafasi kadhaa za kufunga katika kipindi hicho cha kwanza, huku kocha Timbe akimweka jukwaani Jerryson Tegete aliyefunguliwa jana na uongozi wa Yanga.

Villa Squad walipata pigo dakika ya 57 baada ya mwamuzi Ibrahim Kidiwa kumuonyesha kadi nyekundu, Stamili Mbonde kwa kudanganya baada ya kujiangusha na kupewa kadi ya njano ya pili.

Kocha Timbe aliwatoa Asamoah, Mwape na Shamte na kuwaingiza Rashid Gumbo, Hamis Kiiza na Juma Seif, huku Villa wakimpumzisha Lameck Dayton na kumwingiza Kigi Luseke.

Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa Yanga, ambapo dakika ya 63 Kiiza alifunga bao la tatu kwa mabingwa hao akiunganisha pasi ya Rashid ambaye ameonyesha soka ya kiwango cha juu katika mechi hiyo.

Villa Squad walipata bao la pili kwa shuti la mita 20 lililopigwa na Luseke, baada ya mabeki wa Yanga kuzubaa kuokoa mpira katika dakika ya 72 na kumwacha kipa Berko asijue la kufanya.

MWANZA; Kanda ya ziwa kumeonekana kuwa kugumu kwa vinara wa ligi Simba kufuatia kulazimisha sare nyingine ya mabao 3-3 baada ya ile ya 1-1 waliyopata mwishoni mwa wiki dhidi ya Kagera Sugar.

Katika mechi hiyo mshambuliaji Felix Sunzu alifunga mabao mwili peke yake, lakini hayakutosha kuipa pointi tatu Simba mbele ya Toto African kwenye uwanja CCM Kirumba.

Sunzu alifungia Simba bao kwanza katika dakika ya 7, kabla ya wenyeji Toto Afrika kuamka na kusawazisha na kupata bao la kuongoza mabao yote mawili yakifungwa na Enyema Darlington.

Mzambia Sunzu alipachika bao la pili Simba na kusawazisha akimalizia kazi nzuri ya Emmanuel Okwi, lakini Toto walifunga bao la tatu kupitia Soud Mohamed kabla ya Patrick Mafisango kuwasawazisha vinara hao na kufanya timu hizo kugawana pointi.

Mchezo huo ulishuhudia matukio kadhaa katika dakika ya 15 mashabiki walivunja geti la uwanja na kuingia uwanjani, lakini polisi waliweza kuthibiti tukio hilo kabla ya mbwa wa polisi kumponyoka askari na kuingia uwanjani na kuanza kukimbiza wachezaji na alimfukuza zaidi Haruna Moshi na kusababisha mpira kusimama kwa dakika tano katika dakika ya 29.

Pia katika mechi hiyo Simba ilipata pigo baada ya nyota wao Sunzu kuumia na kupoteza fahamu katika dakika ya 42 na kukimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.

TANGA, Mshambuliaji John Boko ameendeleza makali yake ya kuzifumania nyavu baada ya kuifungia Azam bao la kuongoza katika dakika 32 kwa kupiga penati iliyopanguliwa na kipa wa Coastal Union, Omari Hamis na kurudi uwanjani ambako aliuwahi na kumaliza kwa kichwa na kufunga bao hilo.

Mwamuzi Ronald Swai wa Arusha alitoa penati kwa Azam baada ya Boko kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Soud Juma wa Coastal Union na kufanya matokeo kuwa 1-0 hadi mapumziko.

Jinamizi la kukosa penati liliendelea kuiandama Coastal Union baada ya mkwaju wa Mohamed Ibrahim kupanguliwa na kipa Mwidadi Ally wa Azam kufuatia mshambuliaji Ben Mwalala kuchezewa vibaya kwenye eneo la hatari na beki Waziri Salum wa Azam dakika ya 68.

Wakati huohuo, Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara inaendelea tena leo kwenye viwanja vitatu tofauti, ambapo kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, JKT Ruvu watavaana na Moro United, huku kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma, wenyeji Polisi Dodoma watawakaribisha Mtibwa Sugar na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa JKT Oljoro.

Kwenye uwanja wa Chamazi, JKT Ruvu wanaoshika nafasi ya nne wakiwa na pointi kumi wanashuka kwa lengo moja tu la kusaka ushindi dhidi ya Moro United yenye machungu ya kuchapwa mabao 5-2 na Polisi Dodoma.

Kocha wa JKT Ruvu, Charles Kilinda alisema anaingia uwanjani akiwa na kumbukumbu ya kutoka sare na Toto katika mchezo uliopita hivyo ushindi wa leo ni lazima baada ya majeruhi wake kuwa katika hali nzuri kiafya na kuahidi kuwatumia leo.